Usimamizi wa fedha wakati wa janga la virusi vya Covid-19
By Mwanahiba Mzee ~ Experienced Banker on 27 Apr 2020Finance
Wakati dunia nzima ikiwa ni pamoja na nchi yetu ya Tanzania tunapambana na janga la virusi vya Corona linalosababishwa na virusi vya Covid 19, watu wengi wamekuwa wakiulizia hatua bora za kisimamia fedha na uwekezaji wakati pia wakihakikisha afya bora na ulinzi dhidi ya virusi kwao na kwa familia zao. Nimeamua kuandika mambo machache ambayo yanahitaji kuzingatiwa katika nyakati hizi, kutokana na uzoefu wangu kibinafsi na mafunzo kutoka vyanzo mbalimbali:
Kutumia au kuweka akiba
Huu ni wakati wa kuweka akiba, kiasi chochote unachoweza. Watu wanapaswa kutumia kwa hekima kwani waajiri wanatafuta kupunguza gharama kutokana na kupungua kwa kasi ya biashara, janga hili likiendelea, haitoepukika watu kufutwa kazi. Weka akiba, weka akiba, weka akiba. Tumia fedha kwa mahitaji muhimu tu. Chochote ambacho si muhimu kinaweza kusubiri.
Kuwekeza au kuweka akiba
Kama una vyanzo vichache vya fedha, tafadhali weka zaidi akiba na ujizuie kutowekeza kwa sasa. Weka fedha zako katika akaunti ya akiba ambayo haina kizuizi cha utoaji kwani hujui wakati gani utazihitaji.
Ikiwa una ziada kubwa ya fedha , weka kiasi kwenye akaunti ya akiba, na kiasi kwenye akaunti ya amana ya muda mfupi kwani ukwasi ni muhimu zaidi katika nyakati hizi kuliko faida. Pia unahitaji kuwa na uwezo wa kuchukua fursa yoyote ya kuwekeza au kununua mali punde inapotokea kwani kuna watu ambao watakuwa na shida na hivyo wanaweza kuamua kuuza mali (majengo, magari, n.k.) zao kwa bei za chini.
Mikopo
Kwa watu binafsi, hakikisha mikopo yako iko tayari kukusaidia wakati wowote. Hakikisha unapeleka maombi kwa benki au shirika linalokukopesha ili wasitishe malipo ya kila mwezi hadi miezi mitatu. Baadhi yenu tayari mmeshaathirika na janga hili, mmeshaona upungufu katika mauzo ya biashara zenu, maombi ya kupunguza kodi kwa wamiliki wa majengo au tayari mmeshaachishwa kazi. Ni muhimu kuwashirikisha wakopeshaji wenu na kuomba hadi miezi 3 ya usitishaji wa marejesho, sasa.
Ikiwa una amana ya kudumu ambayo haitumiki kama dhamana, ni vyema kuongea na benki yako na kuomba mkopo wa dharura. Kwa wale ambao wana hati fungani za serikali, unaweza kuomba mkopo wa dharura kutoka benki yako na kuweka hati fungani kama dhamana.
Makampuni yahakikishe kuwa yana uwezo wa kukopa kwenye benki zao na wahakikishe kuwa mikopo hiyo iko tayari kutumika wakati wowote fedha zitapohitajika pale ambapo matumizi yatazidi mapato kutokana na kupungua kwa mauzo. Makampuni yanashauriwa kuhakiki uwezo wao wa kulipa mikopo (marejesho ya mwezi, n.k.), na itakapostahili wawashirikishe wakopeshaji ili kusogeza marejesho yao mbele, ikiwezekana waanze kurejesha baad ya miezi mitatu ijayo.
Biashara ndogo ndogo na za kati
Itathmini biashara yako na ufanye marekebisho yanayohitajika ili uendane na fursa na mahitaji ya sasa. Fanya hima kuwezesha biashara yako ili uweze kutoa bidhaa na huduma zinazohitajika kwa sasa kama sabuni za kunawia mikono, Vitakasa mikono, dawa za kusafishia, barakoa, magauni ya kujilinda na maambukizi, n.k. Watoa elimu wanapaswa kujipanga haraka na kuja na elimu kupitia mitandao na kupata njia za kuhakikisha kuwa zinaaminika na kukubalika na mamlaka husika za mitihani. Hoteli, Hosteli, shule, vyuo na wenye sehemu za kuhifadhia mizigo waanze sasa kuongea na serikali na kuwa kwenye hali ya utayari watakapohitajika kusaidia serikali sehemu za karantini. Baadhi ya majengo haya yanaweza kubadilishwa na kutumika kama hospitali za muda au vituo vya afya itakapohitajika.
Usimamizi wa watu
Hakikisha kuwa familia na wafanyakazi wako wako salama kwa kuwapa vifaa vyote muhimu kama inavyopendekezwa na maafisa wa afya wa serikali, kumbuka afya yao ni afya yako. Wagawe wafanyakazi wako kwenye makundi ili wengine wawe nyumbani na wengine wawe kazini, wiki mbili mbili ikiwezekana, ili kuepusha wafanyakazi wote kuwa katika hatari ya maambukizi kwa wakati mmoja. Kwa wale ambao wanaweza kukamilisha kazi yao kutokea nyumbani, wabakie majumbani na wapewe vitendea kazi vinavyohitajika ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.
Wape misaada wafanyakazi wako kwa kuhakikisha mahitaji yao ya mahali pa kazi na ya majumbani mwao yanapatikana ili kuhakikisha wafanyakazi wote wanavuka salama kipindi hiki kwa njia bora iwezekanavyo.
Baki nyumbani, baki salama na ufuate maagizo ya serikali.
Imeandikwa na Mwanahiba binti Mzee ~ Mzoefu katika huduma za kibenki, Tanzania
Kanusho: Maudhui ya makala hii imetokana na uzoefu na fikra binafsi za Mwandishi na sio kwa njia yoyote kuonyesha maoni ya mwajiri wa Mwandishi.